×
New Times Tanzania New Times Tanzania is a multi-media organization with investments in media platforms spanning newspaper print operations, television, radio broadcasting, digital and online services.
New Times Tanzania

WANAFUNZI ZINGATIENI MATUMIZI SALAMA YA MITANDAO YA KIJAMII – MAJALIWA

Na Mwandishi wetu.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa, amewataka wanafunzi nchini kuzingatia matumizi salama na yenye manufaa ya teknolojia ya kidijitali, hususan mitandao ya kijamii, ambayo wengi wao huitumia kupata nyaraka mbalimbali za masomo.

Majaliwa ametoa wito huo leo Jumamosi Juni 14,2025 jijini Dodoma alipokuwa akiongoza maadhimisho ya miaka 21 ya Jumuiya ya Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (TAHLISO), ambapo aliwataka wanafunzi kujiepusha na matumizi mabaya ya mitandao yanayokiuka maadili ya Kitanzania.

“Wanafunzi ni hazina kubwa kwa taifa. Tunategemea mtoe mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi kupitia elimu mnayopata, hivyo ni muhimu kutumia teknolojia kwa njia salama na yenye tija,” amesema Majaliwa.

Aidha, Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea kuboresha elimu ya juu na ya kati kwa kuongeza idadi ya wanafunzi wanaonufaika na mikopo ya elimu ya juu, ili kutoa fursa kwa wengi zaidi kupata elimu.

“Serikali imeongeza bajeti ya mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu, na tutaendelea kufanya hivyo ili kuhakikisha hakuna mwanafunzi anayekosa elimu kwa sababu ya ukosefu wa fedha,” ameongeza.

#NTTupdates