Na Mwandishi wetu.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Kenan Laban Kihongosi leo Julai 1, 2025 amekutana na viongozi wa Dini na mila wa mkoa huo kwa lengo kufahamiana na kupata baraka, dua na maombi kutoka kwa viongozi hao, ili anapoianza kazi yake kama mkuu wa mkoa huo iwe na ulinzi wa Mungu.
Kupitia kikao hicho kifupi, Kihongosi amesema kuwa, anaamini Mhe.Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kumleta Arusha si kwa uwezo wake bali ni mpango wa Mungu, na kuwaomba viongozi hao, licha ya kumpa ushirikiano katika utendaji wake kazi, amewasisitiza kuombea amani ya nchi, kumuombea, kumlea, kumfundisha, kumshauri na kumuelekeza pale panapostahili ili aweze kuitenda kazi vizuri na kuuendeleza mkoa wao wa Arusha.
“Binafsi ninamshukuru Mungu kwa kunipa kibali cha kuja kuwatumikia tena, lakini katika utumishi wa Umma kuna mambo ambayo yanahitaji msaada wa Mungu, hivyo ninaamini ushauri kutoka kwenu kutokana na umri wangu mdogo, niwaombe viongozi wangu msiache kuniombea, ninaombe mnilee mimi ni kajana wenu”. Ameweka wazi Mhe. Kihongosi.
Aidha, amewaomba kuuombea amani ya mkoa huo na Taifa kwa ujumla huku akiwataka kuendeleza ushirikiano wao kama walivyoshirikiana na viongozi waliotangulia katika mkoa huo kwani kilichobadilika ni uongozi na sio mkoa.
Hata hivyo amewasisitiza kendelea kuhubiri amani ya nchi yao, kwa kuangalia manufaa ya amani na utulivu, na kuepuka kujenga chuki na uadui kwa misingi ya dini na vyama kwa kuweke mbele utaifa hususani katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
#NTTupdates.