Na Mwandishi wetu.
Wizara ya Fedha na Mipango imekutana na washirika wa maendeleo kwa ajili ya kutathmini mafanikio na changamoto za utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 na kuweka mikakati ya Dira mpya ya 2050.
Kikao hicho kimefanyika leo Februari 21,2025 jijini Dodoma na kimelenga kujadili namna bora ya kuendeleza miradi ya maendeleo na kuimarisha ushirikiano kati ya serikali na wadau wa maendeleo.
Akiwasilisha hoja katika mkutano huo, Katibu mkuu, ofisi ya Rais fedha na Mipango Zanzibar Dkt. Juma Malik Akil, ameeleza kuwa serikali imefanikiwa kutekeleza miradi mikubwa ya miundombinu ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Ameongeza kuwa ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR ni hatua muhimu katika kuboresha sekta ya usafirishaji, huku miradi mingine kama Bwawa la Mwalimu Nyerere ikitarajiwa kuongeza uzalishaji wa umeme na kuimarisha uchumi wa taifa.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango anayeshughulikia Mipango ya Kitaifa, Dkt. Mursal Milanzi, alisema kuwa majadiliano na washirika wa maendeleo yanalenga kuhakikisha kuwa vipaumbele vya taifa vinaungwa mkono kwa rasilimali na utaalamu unaohitajika.
Akizungumzia mwelekeo wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, amesema kuwa Tanzania ina fursa kubwa ya kukuza uchumi wake kwa kutumia rasilimali zilizopo, ikiwa ni pamoja na kuimarisha sekta ya madini, kilimo, viwanda, na usafirishaji.
Amesisitiza kuwa Dira ya Maendeleo ya 2050 inalenga kuongeza ajira, kukuza uchumi, na kuhakikisha maendeleo endelevu kwa wananchi wote.
#NTTupdates