Na Mwandishi wetu.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema serikali imejipanga kikamilifu kuhakikisha kuwa uchaguzi mkuu ujao wa mwaka huu wa 2025 unafanyika katika mazingira ya amani, utulivu na haki, sambamba na kuiwezesha Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Hayo yamebainishwa na Rais Dkt. Samia wakati akihutubia Taifa leo Aprili 25, 2025, ikiwa ni kuelekea maadhimisho ya miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Katika hotuba yake, Rais Dkt. Samia amesema kuwa mwaka huu wa 61 wa Muungano umeangukia katika mwaka muhimu wa kisiasa, ambapo Watanzania watafanya uchaguzi mkuu wa kuwachagua viongozi katika nafasi mbalimbali.
“Mwaka wa 61 wa Muungano wetu umeangukia kwenye mwaka tunaokabiliwa na jambo kubwa la kidemokrasia nchini.
Tutafanya uchaguzi wa kuwachagua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa Zanzibar, wabunge, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na madiwani,”
Pia, Rais Dkt. Samia amesisitiza kuwa Tanzania itaendelea kudumisha sifa yake kama kitovu cha amani na demokrasia barani Afrika, huku akiahidi kuwa serikali itatoa kila kilichohitajika ili kuhakikisha kuwa uchaguzi huo unakuwa huru na wa haki
“Ni matumaini yangu kuwa tutaendelea kudumisha sifa ya nchi yetu kama kitovu cha amani na cha kidemokrasia iliyojengeka juu ya misingi ya uhuru na haki,”
“Serikali imejipanga kuhakikisha kuwa mahitaji yote ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi yanapatikana kwa ukamilifu na kwa wakati. Tutafanya kila tuwezalo kuhakikisha kuwa uchaguzi unafanyika kwenye mazingira ya utulivu na amani katika kipindi chote cha matayarisho hadi wakati wa uchaguzi,”
Rais Dkt. Samia ameyasema hayo ikiwa ni sehemu ya ujumbe wa kitaifa kuelekea kilele cha maadhimisho ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Aprili 26, 2025, ambapo Watanzania wanatafakari mafanikio ya zaidi ya nusu karne ya mshikamano na maendeleo ya pamoja.
#NTTUpdates