Na Mwandishi wetu.
Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais – Utumishi na Utawala Bora, Bw. Musa Magufuli, ametoa maagizo kwa wizara na mamlaka za serikali kuhakikisha utekelezaji wa mwongozo wa kudhibiti VVU, UKIMWI na magonjwa sugu yasiyoambukiza mahala pa kazi unafanyika kikamilifu ifikapo mwaka 2024.
Akizungumza kwenye kikao cha kitaifa cha waratibu wa afua hizo jijini Mwanza, Magufuli alieleza kuwa ni jukumu la wizara na Sekretarieti za mikoa kuhakikisha mafunzo yanatolewa kwa watumishi, kamati za utekelezaji zinaanzishwa au kuhuishwa, na waratibu wanateuliwa na kupewa vitendea kazi sambamba na kuwasilisha takwimu kwa OR-UTUMISHI.
Magufuli alifichua kuwa hadi mwaka 2025, jumla ya watumishi 1,983 walikuwa wamejiweka wazi kuishi na VVU kutoka taasisi 240, huku 18,842 wakipatiwa huduma za afya ya akili kati ya Julai 2023 na Juni 2025, hali inayodhihirisha changamoto za kiafya kwa watumishi.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Bw. Balandya Elikana, alisema mkoa huo umeunda kamati za kushughulikia afua hizo kuanzia ngazi ya kata hadi wilaya, ingawa anakiri kuwa bajeti finyu imekuwa changamoto kubwa katika utekelezaji wa mipango hiyo.
Balandya aliongeza kuwa ukosefu wa afya njema huathiri uzalishaji, kwani wananchi wengi hujikuta wakitumia muda mwingi kumuuguza wagonjwa badala ya kushiriki kwenye shughuli za kiuchumi kama kilimo, uvuvi na ufugaji, hivyo elimu ya tabia salama inaendelea kutolewa kwa jamii.
#NTTupdates