
Na Mwandishi wetu.
TUME ya Taifa ya uchaguzi(NEC) imeboresha vifaa vya uandikishaji na uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura kutoka kwenye BVR kubwa iliyokuwa na kompyuta ambayo ilikuwa inabeba taarifa za wapiga kura pekee hadi kwenye Kishikwambi ambacho kinabeba taarifa zote za wapiga kura ikijumuisha vifaa vingine kama kamera na (Document Scana).
Hayo yamebainishwa na Afisa TEHAMA Mkuu kutoka Tume ya Taifa ya uchaguzi (NEC) Bw. Lazaro Madembwe, wakati alipokuwa akielezea mifumo ya tehama ya BVR na OVRS katika Kituo cha uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura Shule ya Sekondari ya wasichana Tabora iliyopo Kata ya Ng’ambo Mkoani Tabora.
Amesema katika uboreshaji wa majaribio Tume inatumia teknolojia ya (Biometric) kuandikisha wapiga kura,ambapo huchukua alama za vidole ili kuweza kuwatambua wapiga kura walioandikishwa zaidi ya mara moja na kuondoa taarifa za waliojirudia ambazo ziko kwenye daftari.
“Teknolojia hii ilitumika kwa mara ya kwanza kwa uandikishaji mwaka 2015 na uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura mwaka 2019 na 2020 na vifaa vilivyotumika ilikuwa ni BVR ambayo ilikuwa na Laptop na Camera ambavyo vilikuwa vinakaa tofauti tofauti lakini kuelekea uboreshaji unaofanyika sasa vifaa vyote vinakaa kwenye Kishikwambi ambapo unaskani Nyaraka na kupiga picha kwa kutumia kishikwambi”, amesema Madembwe
Amesema Tume imejitahidi s kupanua wigo wa huduma hapo awali mpiga kura ilikuwa ni lazima afike kituoni kwa ajili ya kuboresha taarifa zake, lakini hivi sasa mpiga kura anaweza kuanzisha mchakato wa awali wa kuboresha taarifa zake kupitia kwenye simu janja au kopyuta iliyounganishwa na intaneti na baada ya hapo atapokea ujumbe mfupi wenye kumbukumbu namba ukimtaka kufika kituoni kwa ajili ya kukamilisha taarifa zake.
“Mfumo huu unaendeshwa kwenye programu wezeshi ambayo ni (Android) ukilinganisha na mwaka 2015,2019 na 2020 ilikuwa inaendeshwa na (Windows) , programu ya Sasa ni nyepesi na ina uwezo wa kuchakata taarifa za wapiga kura kwa haraka zaidi”
#NttUpdates


