×
New Times Tanzania New Times Tanzania is a multi-media organization with investments in media platforms spanning newspaper print operations, television, radio broadcasting, digital and online services.
New Times Tanzania

IDADI YA VIFO VYA AJALI YA MOTO SAME YAFIKIA 42

Na Mwandishi wetu.

Idadi ya watu waliopoteza maisha katika ajali ya mabasi mawili kugongana na baadaye kushika moto wilayani Same, mkoani Kilimanjaro, imeongezeka na kufikia 42, kutoka 39 vilivyoripotiwa awali.

Akizungumza na waandishi wa habari Jumatano, Julai 2, 2025, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, amesema kuwa kati ya waliopoteza maisha, 31 walikuwa wakisafiri katika basi dogo aina ya Coaster, huku wengine 11 wakiwa kwenye basi kubwa.

Kuhusu hali ya majeruhi, Babu amesema jumla ya watu 24 waliokuwa wamelazwa tayari wameruhusiwa kurudi nyumbani baada ya hali zao kuimarika, huku majeruhi wawili wakiendelea kupokea matibabu hospitalini.

Sambamba na hilo, Babu amesema kuwa miili saba kati ya ile iliyonusurika kuteketea kwa moto imetambuliwa na ndugu zao bila ya kuhitaji vipimo vya vinasaba (DNA), na tayari taratibu za mazishi zimefanyika.

“Tunatarajia kupata majibu kamili ya vipimo vya DNA ifikapo jioni ya leo, jambo ambalo litatoa fursa kwa ndugu wa waathirika kuweza kuwatambua wapendwa wao waliopoteza maisha,” amesema.

Ajali hiyo iliyotokea tarehe 28 Juni , 2025 imehusisha jumla ya abiria 67, ambapo 64 walikuwa watu wazima na watoto watatu.

Hata hivyo imebainika kuwa Chanzo Cha kutokea ajali hiyo ni kupasuka kwa tairi la mbele la basi kubwa la abiria kampuni ya Chaneli one jambo lililopelekea dereva kukosa mwelekeo.

#NTTupdates.