Na Mwandishi wetu.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amezitaka Taasisi za kisekta kushirikiana kutekeleza maagizo ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoyatoa katika kikao kilichofanyika machi 24, 2025 ya kuhakikisha wanamaliza changamoto ya magugu maji katika ziwa victoria haraka iwezekanavyo.
Mkuu wa Mkoa ametoa rai hiyo mapema leo Aprili 28, 2025 alipotembelea eneo la Kigongo Ferry, Wilayani Misungwi lililoathirika na Gugumaji Jipya (Salvina Species) ambapo naye ameshiriki zoezi la utoaji magugu maji.
Mhe. Mtanda amesema utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu si la watu wa Bodi ya maji Bonde la ziwa viktoria bali hata Taasisi zingine kama vile Uvuvi kwa kuwa shughuli za uvuvi na ufugaji wa samaki zinafanyika katika ziwa hilo na Ujenzi kwa kuwa kuna shughuli za usafirishaji wa abiria kwa vivuko lakini pia Taasisi za Mazingira pia.
“Hapa kuna athari mbalimbali na sote tunahitajika katika kufanya usafi ziwani, hii shughuli sio ya Bonde tu bali Taasisi na Wizara zingine zinaweza kuathirika lazima muwekeze fedha ili shughuli hii iende vizuri”.
Aidha Mkuu wa Mkoa ameishukuru Serikali kupitia Waziri Mkuu kwa kutoa maelekezo kwa Wizara ya fedha kutoa kiasi cha shilingi Bilioni 3 kwa ajili ya kuimarisha huduma katika ziwa viktoria ikiwemo ununuzi wa mtambo wa uvunaji wa magugu maji katika ziwa viktoria.
“kuwa na mashine ya kisasa ya kufyeka magugu halikwepeki kwa taifa linalotaka maendeleo na kutatua changamoto hii kwa muda mrefu hivyo tunaipongeza sana Serikali”
Naye Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la ziwa Viktoria Dkt. Renatus Shinhu amesema mpaka sasa tayari tani 441 za magugu maji yameopolewa na shughuli hiyo inaendelea ikiwa ni mpango wa muda mfupo mpaka pale mtambo wa kuvuna magugu maji utakapofika kwa kuwa tayari andiko la kupata fedha limeshawasilishwa Wizara ya Fedha kwa utekelezaji.
Changamoto ya magugu maji imekuwa na athari mbalimbali kwa wananchi ambapo shughuli nbalimbali zimekuwa zikiathirika kama vile shughuli za kiuchumi, kijamii, uvuvi na usafirishaji Hivyo kupatikana kwa mashine hiyo ya uvunaji itakwenda kusaidia kutatua na kumaliza changamoto hiyo.
#NTTUpdates